esi dhidi ya JamiiForums: Shahidi adai Polisi hawana utaalamu wa kulazimisha kuingilia mawasiliano kimtandao
Leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, kesi namba 457 ya Jamhuri dhidi ya JamiiForums imeendelea mbele ya Hakimu Godfrey Mwambapa.
Katika kesi hii, kampuni za CUSNA Investment na Ocean Link zilizotuhumiwa na wadau hapa JF kukwepa kodi bandarini zilitaka data za wateja waliofanya hivyo na Uongozi wa JamiiForums ukakataa kufanya hivyo.
Upande wa Jamhuri umeongozwa na Wakili Msomi Batilda Mushi aliyeambatana na wenzake akiwemo Wakili Mutalemwa Kishenyi, Paul Kadushi na Simon Wankyo.
Upande wa JamiiForums, umesimamiwa na Wakili Peter Kibatala aliyeongozana na wenzake Jeremiah Mtobesya na Hassan Kiangio.
Katika kesi hii, Shahidi wa upande wa Jamhuri, Inspekta Msaidizi Monica Pambe toka Jeshi la Polisi Kitengo cha Makosa ya Mtandao (Central Police) na anamekula kiapo kuwa atasema ukweli na ukweli mtupu.
ILIVYOKUWA:
Wakili wa Serikali Batilda Mushi alimtaka Shahidi kujitambulisha na kutaka aeleze kwa ufupi juu ya uzoefu wake kazini (majibu yake yameandikwa kwa kifupi kidogo)
SHAHIDI (Inspekta Monica): Nafanya kazi Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Dar iliyopo Central. Ninafanya kazi kama mpelelezi toka mwaka 2010. Majukumu yangu ni kusikilizia malalamiko toka kwa raia vilele kupelelza mashauri pamoja na kuyafikisha mahakamani.
Wakili wa Serikali: Tujuze elimu na ujuzi umepata wapi
SHAHIDI: Elimu ya upelelezi nimeipata chuo cha mafunzo Moshi 2004-2005. Job training na mafunzo ya makosa ya upelelezi ya kimtandao niliipata ndani na nje ya nchi.
Wakili wa Serikali: Tarehe 16/05/2016 Ulikuwa wapi?
SHAHIDI: Nilikuwa ofisini nikiendelea na kazi, nilipokea jalada la uchunguzi DSM/Z/CID/PE/212215
Wakili wa Serikali: Lilikuwa linahusiana na na kitu gani?
SHAHIDI: Lilikuwa linahusiana na malalamiko ya CUSNA investment na Ocean Link. Walikuwa wanalalamika kuna taarifa kwenye mtaandao wa JamiiForums kwamba kampuni hizo zinahusika na ukwepaji kodi pamoja na kugushi nyaraka za kutoa mizigo bandarini, hivyo waliamini taarifa hizo zinachafua kampuni yao.
Wakili wa Serikali: Je aliyelalamika alisema nani katoa taarifa hizo?
SHAHIDI: Alisema Kwayu JF expert pamoja na Amrish Puri
Wakili wa Serikali: Alielezea taarifa ilitumwaje?
SHAHIDI: Waliipost kwenye mtandao wa JamiiForums. JamiiForums ni mtandao wa kijamii ambapo watu wanawasiliana mambo mbalimbali ya kiuchumi.
Wakili wa Serikali: Wewe kama mpelelezi baada ya kupokea jalada ulifanya nini?
SHAHIDI: Nilielekezwa niandike barua kwenda kwa Mkurugenzi wa JamiiForums, Ndg.Maxence Melo ili kupata taarifa ya aliyeandika kupitia JamiiForums ili tuweze kumhoji kupata ukweli wa jambo hilo. Niliandaa barua baada ya kuandaa barua 10/05/2016 niliipeleka kiongozi wangu kwaajili ya kuipitia na kuisaini na vilevile kuifilisha ofisi husika. Barua niliielekeza kwa Mkurugenzi wa JamiiForums. Baada ya kumpatia kiongozi wangu aliisoma na kuisaini baada ya hapo tullimpigia simu mmoja wa wafanyakazi wa JamiiForums namtambua kwa jina la Chrispine Muganyizi na alifika Ofisini kupokea barua.
Wakili wa Serikali: Alipokeaje barua hiyo?
SHAHIDI: Aliweka sahihi. Kulikuwa na barua mbili, yao na nakala yetu 11/05/2016. Zote aliweka sahihi.
Wakili wa Serikali: Baada ya kuifikisha kwa wahusika nini kilifuata?
SHAHIDI: Tulifuatilia mara nne.
Wakili wa Serikali: Mahakama ingependa kujua. Je, mlifanikiwa kupata majibu. Ufuatiliaji mlifanya kwa nani?
SHAHIDI: Tulifuatilia kwa Mkurugenzi Maxence Melo ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya JamiiForums. Hatukufanikiwa kupata tulichotaka kwake kwa maana ya kwamba hatukujibiwa na athali zake hatukuendelea na Uchunguzi.
Wakili wa Serikali: Baada ya kukwama ulichukua hatua gani kama mpelelezi?
SHAHIDI: Niliwaambia Viongozi wangu kwamba hatukupata taarifa/majibu ya barua. Tukapewa maelekezo tufungue jalada lingine linalohusu kushindwa kutoa vielelezo.
Wakili wa Serikali: Madhumuni ya kufungua faili jipya yalikuwa ni yapi?
SHAHIDI: Lile la kwanza ni la uchunguzi hili lingine ni jinai lenye kumbukumbu CD/IR/4540/2016
Wakili wa Serikali: Baada ya hapo nini kiliendelea?
SHAHIDI: Viongozi walielekeza atafutwe mhusika wa Kampuni ya JamiiForums kwa ajili ya mahojiano
Wakili wa Serikali: Ulikuwa unamlenga nani kama Mhusika wa Kampuni ya JamiiForums?
SHAHIDI: Mkurugenzi ambaye anasimamia hiyo Kampuni anayefahamika kama Maxence Melo
Wakili wa Serikali: Mahakama ingependa kujua kama jitihada zilifanikiwa
SHAHIDI: Ndio jitihada zilifanikiwa na tarehe 14/12/2016 alipigiwa simu akafika ofisini
Wakili wa Serikali: Aliyefika Ofisini ni nani?
SHAHIDI: Maxence Melo
Wakili wa Serikali: Baada ya kufika nini kiliendelea?
SHAHIDI: Alihojiwa kwa kutokutoa ushirikiano kuhusu mteja wake aliyeandika hizi taarifa kwenye mtandao.
Wakili wa Serikali: Baada ya kumpata na kumhoji mliweza kufanikiwa kupata mlichokuwa mnataka?
SHAHIDI: Hapana, Maxence alisema hawezi kabisa kutoa taarifa wateja wake katika Mtandao wa JamiiForums.
Wakili wa Serikali: Awali nani alimpigia Simu Maxence?
SHAHIDI: Alipigiwa Simu na Inspekta Msangi
Wakili wa Serikali: Baada ya kuona hamkufanikiwa mlifanya nini sasa?
SHAHIDI: Viongozi walisema tuandae jalada tulilete mahakamani kwa kosa la kutokutoa vielelezo.
Wakili wa Serikali: Na huyu mtu anayeitwa Micke William unamfahamu?
SHAHIDI: Namfahamu kama mmoja wa shareholders wa JamiiForums
Wakili wa Serikali: Umeongelea kuhusu Maxence Melo, ukimuona mahakamani unaweza kumtambua?
SHAHIDI: Namfahamu, huyu hapa(anaenda na kumshika bega.. Huyu hapa)
Wakili wa Serikali: Je, Micke yupo?
SHAHIDI: Yupo pia(anaenda na kumshika bega.. Huyu hapa)
Wakili wa Serikali: Je, una majukumu mengine baada ya kumfikisha mahakamani?
SHAHIDI: Baada ya kumfikisha mahakamani hakuna jukumu lingine zaidi ya kufuatilia Kesi
AKAINGIA WAKILI WA WASHTAKIWA, Ndg. KIBATALA:
Kibatala: Lile jalada la kwanza bado mnaendelea nalo?
SHAHIDI: Tuliliweka pending kwanza, Nilikiwa nashirikiana Inspekta Peter(wa kitengo cha Makosa ya Mtandao)
Kibatala: Tuanishie jalada ambalo wewe ulipewa na jalada unalotuelezea sisi
SHAHIDI: Jalada la awali ni jalada la uchunguzi, bado hatujapata ushahidi wa kutosha na malalamiko yale hatujaridhika nayo kwanza. Kama tukijiridhisha tutafungua kesi
Kibatala: Tofauti na hili la leo ni nini?
SHAHIDI: Hili tuliloleta mahakamani ni kosa tofauti na lile tulilokuwa tunapeleleza. Hii inahusu Mkurugenzi wa JamiiForums kutokuta taarifa za wateja ambazo zingetusaidia kufanya upelelezi
Kibatala: Kwenye hiyo kampuni, ni nani ambaye angepaswa kutoa ushirikiano?
SHAHIDI: Tunaamini kwenye kampuni kunakuwa na kiongozi na kwenye hii kesi Kiongozi
Kibatala: Tusaidie, hizi kampuni ulizozitaja zimekashifiwa kijinai au kimadai?
SHAHIDI: Kijinai
Kibatala: Na hilo ni hitimisho lako la kipelelezi?
SHAHIDI: Hatujahitimisha
Kibatala: Umesoma sheria kidogo?
SHAHIDI: Hapana sijasoma
Kibatala: Ulisema hizo kampuni zililalamika kuwa zimechafuliwa; je, hizo tuhuma ni za kweli au sio za kweli?
SHAHIDI: Hatujui kama ni kweli au si kweli
Kibatala: Kama hujui kama ni kweli au si kweli. Je, kupost Peter Kibatala ni wakili ni kosa?
SHAHIDI: Hapana, si kosa kupost kitu cha kweli
Kibatala: Shahidi unasema ulimpigia simu Chrispine Mganyizi, namba zake ni zipi? Maana umekuja hapa ukataja namba za mafaili yote, ni wazi una kumbukumbu nzuri.
SHAHIDI: Sina uhakika wa namba
Kibatala: Nani alifanya shughuli za kufanya za kujua wakurugenzi wote ni wa kampuni?
SHAHIDI: Mimi na Peter
Kibatala: Baada ya kujiridhisha hawa directors wa JamiiForums; Je, una nyaraka za kisheria kuthibitisha hilo?
SHAHIDI: Zipo tulizitoa Brela
Kibatala: Shahidi umesema uliandika barua na sahihi mkubwa wako; ni nani?
SHAHIDI: Anaitwa ASP Fadhili Bakari
Kibatala: Nakupa barua (akampa) naomba umuambie hakimu kama ndo wewe uliandika
(Anaangalia barua na kusema ni Yenyewe aliyoiandika)
Kibatala: Hivyo vifungu vya sheria ulivinukuu wewe au boss wako?
SHAHIDI: Aliandika boss wangu, alinielekeza
Kibatala: Nataka unisaidie, wewe uliandika kama kasuku au uliandika ukifahamu unachoandika ni nini? Huyu alishitakiwa kwa Cybercrime Act?
SHAHIDI: Nilipoandika barua nilimpelekea boss akaisoma akanambia ingiza kifungu hicho nikaingiza nikampelekea akasaini.
Kibatala: Je, wewe uliandika kama kasuku au unafahamu hicho kifungu?
SHAHIDI: Sikifahamu
Kibatala: Naomba usome hizo sheria mbili umwambie hakimu; je, ni sheria moja au ni sheria mbili tofauti?
SHAHIDI: Sifahamu tofauti
Kibatala: Mimi sijakuuliza kama unafahamu tofauti. Nimekuuliza sheria zinafanana au hazifanani? Mwambie hakimu, Kwa kuangalia hizo Sheria
SHAHIDI: Sheria ya kwenye barua ni Criminal Procedure Act huku kwingine ni Cybercrimes Act
Kitabatala: Mwambie hakimu ni nini kilikufanya ujue Kwayu JF expert pamoja na Amrish Puri ni wateja wa JamiiForums?
SHAHIDI: Kwa sababu ni majina yalionekana yamepost ule ujumbe kweye mtandao wa JamiiForums
Kibatala: Je, Mtandao upo hapa Mahakamani?
SHAHIDI: Hapana
Kibatala: Je, huo mtandao mheshimiwa hakimu kauona?
SHAHIDI: Hapana, lipo kwenye jalada la kesi.
Kibatala: Je wakati mnawaandikia barua JamiiForums, mliwaeleza wajibu kwa namna gani?
SHAHIDI: Kwa namna yoyote waliyoona inafaa
Kibatala: Nakuonesha barua iliyoandikwa 17/5/2016 ikielekezwa kwa mkurugenzi wa Upelelezi kama majibu toka Jamii Media (ina na mhuri wa kupokelewa toka Polisi). Unaifahamu? (anampa barua) Hiyo ilikuwa ni barua ya wakili Benedict Ishabakaki
Jibu: Hii barua sijaipata
Kibatala: Ilipokelewa 27/06/2016 kwa ZCO. Je, huo mhuri ni mhuri ni wa Ofisi yenu?
SHAHIDI: Sina uhakika wa Mhuri lakini ni mhuri wa ofisi ya mkuu wa Upelelezi
Kibatala: Katika ushahidi wako, umesema ulifuatilia mara nne, tuambie ulifuatiliaje? Utaje kwa tarehe mpaka zifikie hizo mara nne
SHAHIDI: Hizi tulifanya tukiwa wawili mimi na Peter
Kibatala: Je, ulifuatilia ngapi? Au zote alyefuatilia ni Peter?
SHAHIDI: Alifuatilia Peter
Kibatala: Shahidi, ulisema ulimpigia simu Maxence na kusema hataweza kutoa taarifa za wateja wa JamiiForums; wewe Ulimwelewaje?
SHAHIDI: Nilielewa yeye kama mkurugenzi hawajibiki na kutoa taarifa.
Kibatala: Wewe kama mpelelezi ulimuelewaje? Hataki, hana utaalamu wa kupata data hizo, analinda faragha za watoa taarifa wake au wewe ulielewaje mpaka ukatoa mashitaka haya?
SHAHIDI: Nilielewa kwamba hatatoa
Kibatala: Hatatoa kwa sababu gani? Mahakama inataka ijue, kwamba alikuwa hataki?
SHAHIDI: Mimi hadi tunafika hapa mahakamani nilielewa kwamba hakutaka kutoa vielelezo
Kibatala: Nani aliandika maelezo ya Maxence alipokuwa mtuhumiwa?
SHAHIDI: Aliandika afande Chrispin
Kibatala: Maelezo yaliyoandikwa na Chrispin uliyasoma?
SHAHIDI: Nliyasoma ila ni kipindi kirefu kidogo
Kibatala: Kwa kumbukumbu zako Maxence alisema nini kwenye maelezo yake Polisi?
SHAHIDI: Sikumbuki.
Kibatala: Shahidi wewe unatoka kwenye Kitengo Maalum cha Kanda Maalum kuhusu Makosa ya Mtandao?
Jibu: Ndio
Kibatala: Nikuulize kipelelezi sasa; Mna utaalamu wa kutosha wa kulazimisha kuingilia mitandao kama JamiiForums (force entry)?. Mfano, mtu anaandika kuwa anapanga kumuua Rais, mnaweza kuingilia mtandao kujua nani anataka kumuua Rais? Namaanisha, Mnao uwezo wa ku-force kuingia kutafuta kujua taarifa binafsi za mhusika (Identity)?
SHAHIDI: Hatuna uwezo huo ila utaalam tunao lakini tuna mipaka
Kibatala: Tunaomba utuambie mipaka hiyo imewekwa na nini au nani, kama ni sheria sema nis sheria ipi!
SHAHIDI: JamiiForums ina Mkurugenzi. Sasa sisi kama tunataka taarifa tunamuomba taarifa
Kibatala: Mkurugenzi wa JamiiForums amegoma, mtakaa msubiri hadi Rais auawe au mta-force kuingilia mtandao mumjue?
SHAHIDI: Tuna mipaka
Kibatala: Narudia - Mnao uwezo wa ku-force entry?
SHAHIDI: Hatuna uwezo wa ku-force entry
Kibatala: Mnafahamu kuwa kuna utaratibu wa kisheria unaowataka kuja mahakamani kuomba mahakama ilazimishe mpewe taarifa mnazotaka toka JamiiForums? Mliiomba mahakama ifanye hivyo?
SHAHIDI: Hatukufanya maombi Mahakamani
Kibatala: Je, unafahamu kwamba mtu akigoma kutoa taarifa sheria inawaruhusu kuomba mahakama imlazimishe mhusika kutoa taarifa?
SHAHIDI: Tunafahamu
Kibatala: Mlipokwenda BRELA mlikuta imesajiliwa inaitwa nini hiyo Kampuni?
SHAHIDI: Anaomba asome BRELA ilikuwa inasomekaje (Amekuta nyaraka hazipo mahakamani)
Kibatala: Je, kisheria JamiiForums na Jamii Media ni Kitu kimoja?
SHAHIDI: Sina la kusema
Kibatala: Maelezo unasema JamiiForums na charge sheet inasema Jamii Media; ni kitu kimoja?
SHAHIDI: Sina la kusema
Kibatala: Je, upelelezi wako ulikuthibitishia kwamba hawa walikataa kwamba ulikuwa unajua wanawafahamu hao walioandika taarifa katika JamiiForums?
SHAHIDI: Sijui kama wanawafahamu au hawawafahamu
Kibatala: Ni nini kilikuthibitishia kwamba Chrispine Muganyizi ni mtu mwenye uhusiano wa kisheria na Jamii Media?
SHAHIDI: Hatukumpa kisheria, tulimpa ili afikishe kwa wahusika
Kibatala: Ni nini kilichokuthibitishia kwamba barua ilifika huko Jamii Media?
SHAHIDI: Ni viongozi wangu walikuwa wanawasiliana nao sio mimi
Kibatala: Ulishawasiliana na TRA au TPA (kujua kama CUSNA Investment walikuwa wakwepa kodi)?
SHAHIDI: Hapana
Wakili: Mlifanya mawasiliano na TCRA?
SHAHIDI: Sina uhakika
WAKILI KIBATALA AKAMWACHIA WAKILI MTOBESYA:
(Wakili Mtobesya anasema atauliza maswali machache)
Mtobesya: Ulisema kuna jalada mlifungua la kushindwa kutoa ushirikiano si ndio?
SHAHIDI: Ndio?
Mtobesya: Hadi mnafungua jalada la Upelezi si mnaona kwamba kuna kifungu kimevunjwa?
SHAHIDI: Ndio
Mtobesya: Mwambie hakimu kifungu mlichokiweka ni kipi? Kilichokuja mahakamani mlichoandika kwenye barua?
SHAHIDI: Mahakama ndo inatafsiri sheria
Hakimu Mwambapa: Mara ya kwanza mlisema mliweka kifungu cha sheria na mara ya pili unasema hamkuweka. Sielewi. Barua mlitumia Criminal Procedure Act na Mahakamani mkaja kwa kifungu kingine si ndio?
Shahidi anaonekana kukosa majibu...
Mtobesya: Mliomba taarifa chini ya sheria gani?
SHAHIDI: Chini ya kifungu cha kumi Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA)
Mtobesya: Wewe ni mmoja wa wapelelezi?
SHAHIDI: Ndio
Mtobesya: Katika upelelezi wako, uliweza kufahamu taratibu zinazowaongoza wanachama wa JamiiForums katika kuchangia mijadala mbalimbali?
SHAHIDI: Sheria zinazoongoza mijadala kwa wateja wa JamiiForums sizifahamu
Mtobesya: Je, ulifahamu ni katika mazingira gani hizo taarifa nyeti za watumiaji wa mitandao zinaweza kutolewa?
SHAHIDI: Sifahamu
Mtobesya: Unafahamu kwamba katika nchi hii mtu ana ulinzi wa mawasiliano yake kisheria?
SHAHIDI: Ndio
Mtobesya: Unafahamu pia ni katika mazingira gani ulinzi huo unaweza usiwepo?
SHAHIDI: Ndio nafahamu
Mtobesya: Wakati unapeleleza, ni nini hasa mlichotaka kuthibitisha(verify)?
SHAHIDI: Hatukutaka ku-verify, tulitaka tuwahoji kama zile taarifa ni za kweli au sio za kweli ili tu-take action. Lengo la kwenda JamiiForums ni kutaja kuwaapata wale walioleta taarifa. Hatuwezi kuwapata bila kuwauliza wahusika wa JamiiForums.
Mtobesya: Taarifa zimetolewa kwamba hawa watu wamekwepa kodi, wenye ku-verfy ni TRA au hawa walioandika?
SHAHIDI: Sisi tulitaka kuwahoji hawa walioandika
Mtobesya: Hivi, mlikuwa mnachunguza nini?
SHAHIDI: Uchunguzi unaweza kubaini mambo mengi sana. Malalamiko toka CUSNA yalikuwa ni kuwa kampuni imechafuliwa sio kukwepa kodi
Mtobesya: Je, mlichokuwa mnachunguza ni hayo makampuni ya CUSNA Investment na Ocean Link kuchafuliwa au kukwepa kodi?
SHAHIDI: Tulikuwa tunachunguza suala la kuchafuliwa.
Mtobesya: Je, ulikwenda TRA kuuliza kama walikwepa kodi?
SHAHIDI: Hapana
Mtobesya: Unakumbuka TPA iliwahi kutoa orodha ya Makampuni yaliyodaiwa kukwepa kodi bandarini Dar es Salaam?
SHAHIDI: Ndio, nakumbuka
Mtobesya: Je, sahihi nikisema CUSNA Investment ni moja ya makampuni yaliyokwepa kodi?
SHAHIDI: Inawezekana
Mawakili wa upande wa utetezi (JamiiForums) wanateta na kuamua kuacha kuendelea kumhoji shahidi...
========
Wakili wa Serikali: Mheshimiwa(hakimu), hatuna shahidi mwingine kwa siku ya leo.
Kesi itatajwa tena tarehe 20/09/2017
Comments
Post a Comment